Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni taasisi ya serikali ya Tanzania inayosimamia utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu. Ilianzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi kutoka familia zenye kipato kidogo, ili kuhakikisha kwamba masomo yanapatikana kwa wote bila kujali hali ya kiuchumi. HESLB inajikita katika kutoa mikopo ambayo inasaidia kugharamia ada za shule, vitabu, na gharama nyingine zinazohusiana na masomo.
Mikopo inayotolewa na HESLB inategemea kanuni na masharti maalum, ambapo wanafunzi wanatakiwa kuomba kwa njia rasmi. Kila mwaka, bodi inafanya mchakato wa kuchambua maombi na kuamua ni wanafunzi gani watafaidika. Aidha, bodi inatoa mwongozo wa jinsi ya kulipa mikopo hiyo baada ya kumaliza masomo, ambapo walengwa wanatakiwa kurejesha mikopo yao kwa asilimia fulani ya mapato yao. Hii inasaidia katika kuhakikisha kuwa mfumo wa mikopo unakuwa endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia amesema wanafunzi wote walioomba mikopo kwa mwaka 2024/2025 wanaweza kupata taarifa za kina kuhusu mikopo yao kupitia akaunti walizotumia kuombea mikopo maarufu kama ‘SIPA’ – Student’s Individual Permanent Account.
“Leo tumeanza kutoa taarifa za mikopo kwa makundi yote, waliopangiwa mikopo, wapo ambao bado tunaendelea kufanyia kazi maombi yao … kila mwombaji anapata taarifa yake kwenye akaunti ile ile aliyotumia kuombea mkopo, huhitaji kufika ofisi za HESLB”, amesema Dkt. Kiwia na kuongeza kuwa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na shahada ya Uzamivu unaendelea.
Dkt. Kiwia amesema HESLB imeanza kuandaa malipo ya wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo ambao ni wanufaika wa mikopo na kusema lengo ni kuhakikisha fedha zinafika vyuoni kwa wakati.
“Mwaka huu, Serikali imetenga TZS 787 bilioni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 245,799 wakiwemo zaidi ya wanafunzi 88,000 wa mwaka wa kwanza waliotengewa TZS 284.8 bilioni,’ amesema Dkt. Kiwia na kuongeza kuwa bajeti ya mwaka 2024/2025 imeongezeka kwa TZS 38 bilioni sawa na asilimia 5.1 ikilinganishwa na bajeti ya 2023/2024 iliyokuwa TZS 749.4 bilioni. Mwaka huu pia kiwango cha chini cha mkopo kwa mnufaika mmoja mmoja kimepanda hadi TZS 3.0 milioni kutoka TZS 2.7 milioni mwaka uliopita wa 2023/2024.
Kuhusu wajibu wa vyuo, Dkt. Kiwia amevikumbusha vyuo ambavyo havijawasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi-wanufaika wanaoendelea na masomo, kuwasilisha ili kuiwezesha HESLB kuandaa malipo kwa wakati.
“Kuna vyuo vichache, ambavyo bado havijawasilisha matokeo, tumewakumbusha na tunasisitiza waharakishe kuwasilisha matokeo ili tukamilishe malipo ya wanafunzi waliofaulu kuendelea na masomo,” amesema Dkt. Kiwia.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB amesema kuwa awamu ya pili ya orodha ya wanafunzi waliopangiwa mikopo kwa mwaka 2024/2025 itatangazwa wiki ijayo